Pages

Thursday

Mazungumzo ya kuleta amani nchini Somalia yamemalizika na kutoa makubaliano kwa pande zote kujituma na kujitolea kuijenga upya nchi ya Somalia

 Rais wa Somalia Sheikh Sharif Sheikh Ahmed (kati) akipeana mkono na mwakilishi maalumu wa Umoja wa Mataifa kwa Somalia, Augustine P.Mahiga
                                    imeandikwa na sauti ya amerika

Makundi makuu ya kisiasa nchini Somalia yalimaliza mazungumzo yao ya siku tatu mjini Addis Ababa Ethiopia  Jumatano kwa kusema kuwa yamejitolea kuona mchakato wa amani wa mabadiliko ya kiutawala nchini mwao ifikapo  mwezi Agosti mwaka huu.

Washiriki wa mkutano huo uliodhaminiwa na Umoja wa Mataifa walionyesha muungano usio wa kawaida huku kukiwa na masuala tete ya kujadiliwa ambayo kwa kawaida huwa magumu kuyajadili baina ya koo mbalimbali zinazozozana huko Somalia. Mwishowe vyama vyote sita vilikubaliana  kuweka kando masuala mengi mazito pamoja na yale madogo madogo kwa maslahi ya kuwa na serikali thabiti baada ya siku 90 ambapo  utawala wa serikali ya mpito ndipo utakapofunga shughuli zake.

Waziri mkuu wa serikali ya mpito Abdiweli Mohammed Ali ambaye anaonekana kuongoza juhudi za  kile kinachoitwa mkakati mpya wa ratiba kuelekea utawala mpya alisema motisha kwake inatokana na mapenzi ya kuona mzozo wa Somalia umeisha na taifa hilo limeondolewa kwenye orodha ya nchi zilizoshindwa kabisa kuwa na uthabiti wa kisiasa.Makubaliano yaliyotiwa saini Addis Ababa Jumatano  baada ya mazungumzo kumalizika yanazitaka pande zote husika kujituma  na kujitolea kuijenga upya Somalia.

Makubaliano hayo pia yanatoa mwito kuwe na bunge katika muda wa mwezi mmoja na katiba ya muda ifikapo Julai 10 ambayo itafuatiwa na kuapishwa kwa wabunge siku 10 baadaye na kukamilisha kipindi cha serikali ya mpito kabla ya tarehe ya mwisho ya Agosti 20 ambapo serikali ya mpito inatakiwa kumaliza ramsi shughuli zake.

Rais wa serikali ya mpito Sheikh Sharif Sheikh Ahmed ambaye huenda akapoteza wadhifa wake huo baada ya hatua hizo kutekelezwa alisifu mwamko mpya wa umoja na ushirikiano miongoni mwa makundi mbalimbali na koo ambazo kihistoria zimekuwa zikizozana nchini Somalia.

No comments:

Post a Comment