Iran na Mataifa sita yenye nguvu duniani wanasaka mapatano ya 
mpango wa nyuklia wa nchi hiyo leo mjini Baghdad huku kukiwa na 
matumaini ya kukififisha kile ambacho Rais Barack Obama amekiita kuwa ni
 "kitisho cha vita" .
       
 Kiini cha majadiliano hayo ni hofu juu ya miradi ya nyuklia ya Iran 
ambayo mataifa hayo yanaishuku kuwa ni mwanzo wa kulekea kwenye 
utengenezaji wa silaha za atomiki ingawa nchi hiyo imekanusha na kusema 
kuwa mpango wake huo ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida.
 Mataifa ya magharibi yana wasiwasi huenda nchi hiyo ikazidi kuvuruga 
amani kwenye nchi za Mashariki ya Kati ambazo tayari ziko katika hali 
mbaya kutokana na machafuko ya mara kwa mara, pamoja na kuzizika juhudi 
za kimataifa za kuzuia utengenezaji wa silaha za nyuklia zinazoendeshwa 
kwa miaka 60 sasa.  
 Viongozi wanaoshirki mkutano huo wamepaza sauti zao wakiitahadharisha 
Iran kutokuvuruga mazungumzo hayo, lakini pia wakiahidi kuwa tayari 
kuisaidia nchi hiyo kusonga mbele endapo itaonyesha ushirikiano na 
kuuweka wazi mpango wake wa nyuklia.
 Shabaha kuu kwenye majadiliano hayo ni kuifanya Iran ipunguze kiwango 
cha urutubishaji wa madini ya Uranium pamoja na kuruhusu Shirika la 
Kimataifa la Nguvu za Atomiki, IAEA,  kuvikagua vinu vyake vya nyuklia 
kikiwemo cha Puchin kama alivyoeleza Mkuu wa shirika hilo Yukia Amano
 Kundi hilo linaloongozwa kwenye mazungumzo hayo na Mkuu wa Sera za 
Kigeni wa Umoja wa Ulaya Catherine Ashiton, linatarajia kutoa matakwa 
yake kwa Iran ambayo itawakilishwa na kiongozi wake wa mazungumzo ya 
nyuklia Saeed Jalili ikiwemo suala la kujenga ujasiri.
 Hakuna nia ya kulegeza vikwazo  dhidi ya Iran
 Nchi za magharibi zimesema kuwa hazitarajii kulegeza vikwazo vya 
kiuchumi zilizoiwekea Iran ambavyo vinatajwa kuongeza makali ya 
shinikizo kwa taifa hilo. Mazungumzo ya sasa ni yanafuatia yale 
yaliyofanyika mjini Instanbul  zaidi ya mwezi mmoja uliopita.
 Mazungumzo ya Baghdad yanafanyika muda mfupi baada ya Amano kutangaza 
kuwa IAEA iko mbioni kusaini makubaliano ya ukaguzi wa vinu vya nyuklia 
na Iran.
 Hapo jana Marekani ilitangaza kuiwekea vikwazo vya kiuchumi nchi hiyo 
kama hatua ya kuishinikiza kukubali matakwa ya mataifa hayo juu ya 
mpango wake wa nyuklia vikiongeza idadi ya vile ambavyo tayari 
vimekwishawekwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa pamoja na Umoja
 wa Ulaya.
 Rais wa nchi hiyo Barack Obama ameapa kuendeleza shinikizo hadi hapo mambo yatakapokaa sawa. 
 Iran inarutubisha madini ya Uraniumu kwa kiasi cha asilimia 20 kiwango 
ambacho wataalamu wanasema kuwa ni sawa na asilimia 90 ya urutubishaji 
unaohitajika kutengeneza silaha za nyuklia.
 Wawakilishi wa nchi tano Wananchama wa kudumu wa Baraza la Usalama la 
Umoja wa Mataifa wanaoshiriki mazungumzo hayo yaani Urusi, China, 
Marekani Ufaransa, na Uingereza tayari wanaelekea katika eneo la 
mkutano. Ujerumani pia inashiriki mazungumzo hayo.
 
No comments:
Post a Comment