Habari hii imeandikwa na Tanzania Daima
RAIS Jakaya Kikwete ameanza mchakato wa kuunda Baraza jipya la
Mawaziri linalotarajiwa kutangazwa wakati wowote kuanzia leo huku akitoa
taswira ya kuundwa kwa serikali itakayojumuisha wanasiasa wanaotoka nje
ya Chama cha Mapinduzi (CCM).
Katika hatua ya kwanza, Rais Kikwete amewateua watu watatu wenye sifa
na rekodi tofauti za kisiasa, kiuongozi na kitaaluma kuwa wabunge.
Miongoni mwa wateule hao watatu wapya wa Kikwete waliotangazwa jana ni
Mwenyekiti wa Taifa wa chama cha NCCR-Mageuzi, James Mbatia.
Taarifa fupi ya Ikulu iliyosambazwa jana jioni kwa vyombo vya habari
imewataja wengine walioteuliwa na rais kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania
Ibara ya 66(i) (e) kuwa wabunge wapya ni pamoja na Prof. Sospeter
Muhongo na Janet Mbene.
Kuteuliwa kwa Muhongo ambaye kitaaluma ni bingwa wa masuala ya
jiolojia kuwa mbunge, kunaongeza uwezekano wa kuingizwa katika baraza la
mawaziri akishika moja ya wizara nyeti.
Miongoni mwa wizara ambazo anaweza kushika kuziongoza ni pamoja na
Wizara ya Nishati na Madini ambayo kwa sasa inaongozwa na William
Ngeleja.
Wakati jina la Prof. Muhongo likiwa geni masikioni mwa Watanzania,
uteuzi wa Mbatia ulizua mjadala wa ghafla kutoka kwa watu mbalimbali,
akiwamo mmoja wa wabunge machachari wa NCCR- Mageuzi.
Hii ni mara ya pili kwa Rais Kikwete kuwateua wapinzani kuingia ndani
ya Bunge. Alipata kufanya hivyo wakati alipokuwa akikaribia kumaliza
muhula wake wa kwanza madarakani, wakati alipomteua kiongozi maarufu wa
Chama cha Wananchi (CUF), Ismael Jussa Ladhu, kuwa mbunge.
Mbatia amewahi kuwa mbunge mwaka 1995-2000 kupitia chama hicho katika
jimbo la Vunjo mkoani Kilimanjaro, ambapo katika uchaguzi ulioisha mwaka
2010 aliwania nafasi hiyo katika jimbo la Kawe na kuangushwa na mgombea
wa CHADEMA, Halima Mdee.
Kuteuliwa kwa Mbatia kumefuta minong’ono ambayo ilikuwa ikimtaja
Mwenyekiti wa Taifa wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, kuwa miongoni mwa
wanasiasa wa upinzani ambao walikuwa wakipewa nafasi kubwa ya kuingia
katika serikali mpya ya Kikwete.
Muhongo kitaaluma ni Profesa wa Jiolojia kutoka Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam.
Kwa sasa ni Mhariri Mkuu Mtendaji wa jarida la jiolojia la kanda ya
Afrika na vile vile ni mshirika wa wanajumuiya za kimataifa za
wanataaluma wa jiolojia kama Geological Society of London na Chinese
Academy of Geological Sciences.
Prof. Muhongo pia ni Makamu wa Rais wa Kamisheni ya wanajiolojia wa ramani ya dunia toka mwaka 2005 hadi sasa.
Amehudumu kama mtafiti katika Chuo Kikuu cha Mainze nchini Ujerumani mwaka 2000 hadi 2009.
Mwaka 2009, alikuwa miongoni mwa watu waliopendekezwa kutoka Tanzania
kushika nafasi ya Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa
linaloshughulikia Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO).
Janet Mbene ambaye anateuliwa na Kikwete kwa mara ya pili katika
mihula tofauti kuwa mbunge, ni msomi na mchumi wa ngazi ya juu akiwa
amefanya kazi katika taasisi na mashirika mengi ya kimataifa.
Akiwa mwanzilishi na mkurugenzi wa taasisi ya SIA, inayojihusisha na
kuwajengea uwezo wa kiuchumi kampuni ndogo na za kati hapa nchini, Mbene
amewahi kufanya kazi katika shirika la kimataifa la Oxfam
linalojihusisha kupambana na umasikini, chini ya mradi wa Maendeleo wa
Umoja wa Mataifa na Shirika la Kazi duniani (ILO).
Katika nafasi hizo, Mbene ambaye hivi karibuni alianguka katika
kinyang’anyiro cha ubunge wa Afrika Mashariki, alijikita zaidi kusimamia
miradi ya maendeleo iliyolenga kuwasaidia wajasiriamali na wazalishaji
wa bidhaa, masoko na kusimamia kikamilifu utendaji kazi bora za sekta
binafsi.
Mbene ni mwanzilishi wa taasisi ya Yatima ambayo inalea watoto yatima
ambao wazazi wao wamekufa kwa ukimwi na kupigania haki za yatima.
Aidha alianzisha bodi ya wadhamini ya wanawake wachumi Tanzania, yenye
lengo la kuinua uwezo wa kiuchumi wa wanawake hususan wa vijijini.