Pages

Friday

CCTV kuwekwa miji yote ya Kenya

 Mfano wa kamera zitakazowekwa katika miji ya Kenya ili kupambana na ugaidi na kuimarisha ulinzi
                             imeandikwa na sauti ya amerika
Waziri Mkuu wa Kenya Raila Odinga amesema nchi yake imepokea fedha kutoka China  za kugharamia kamera za  kufuatilia matukio mbalimbali nchini humo katika juhudi za kupambana na ugaidi katika miji ya Kenya.

Bwana Odinga aliliambia bunge la Kenya kuwa katika siku za karibuni serikali itaweka kamera hizo zinazojulikana  kama CCTV kote nchini Kenya kuanzia jiji kuu la Nairobi ikifuatiwa na Mombasa , Kisumu na miji mingine. Alisema  serikali ya Kenya imepokea msaada wa dola milioni 100 kutoka China za kupambana na ugaidi na kuimarisha ulinzi nchini humo.

Lakini katika mitaa ya Nairobi wakenya walikuwa na hisia mbalimbali. Albert Bwire alisema  hiyo ni  dhana nzuri ya kuweka kamera za CCTV  ili kurekodi visa vya uhalifu haswa wakati wa uchaguzi.  Lakini  Jimmy Kariuki alipinga mpango huo akisema hadhani utasaidia chochote. Alihoji kwanini  serikali inalenga miji mikubwa bila kuwafikiria wale waliopo vijijini.

Mkenya mwingine  Alois Gitonga  alieleza wasiwasi wake juu ya uwezekano  wa ufisadi katika mradi huo. Alisema Kenya imekuwa na kashfa nyingi sana. Kwa hiyo hawezi kusema kwa uhakika kwamba mpango huu utafanikiwa ama fedha hizo hazitaishia kwenye mfuko wa mtu.

Serikali ya Kenya imeongeza juhudi zake za kupambana na ugaidi katika miaka ya karibuni ikitilia uzito zaidi jamii kubwa ya wasomali nchini humo  baada ya  mashambulizi  kutoka Somalia kwenye mpaka wake na Somalia, utekaji nyara wa watalii , wafanyakazi wa kutoa misaada na hata askari polisi wa Kenya.

No comments:

Post a Comment