Pages

Tuesday

Miji nchini Afrika Kusini yenye matumaini kupewa fursa kuandaa mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika mwakani, itafahamu kama imepata bahati hiyo tarehe 4 mwezi wa Aprili.

Miji Afrika Kusini yagombea kuandaa Kombe la Afrika
Walitarajiwa kufanya hivyo siku ya Ijumaa lakini waliomba muda zaidi wa kujiandaa.Wale wanaotafuta nafasi katika miji saba, watawasilisha maombi yao kwa kamati ya maandalizi siku ya Jumatatu.
Meneja wa mawasiliano wa Chama cha Kandanda cha Afrika Kusini Dominic Chimhavi, ameongeza kusema maombi yatakayofanikiwa yatatangazwa tarehe 4 mwezi wa Aprili.
Shirikisho la Kandanda la Afrika (Caf) linajipanga kutembelea viwanja nchini Afrika Kusini mwezi wa Aprili.
Uzinduzi rasmi wa michuano hiyo pia umepangwa kuwa tarehe hiyo 4 mwezi wa Aprili.
Tangazo la miji itakayofanikiwa kuandaa mashindano hayo litatolewa mbele ya wajumbe wa Shirikisho la Kandanda la Afrika wakati wa uzinduzi.
Afrika Kusini imepata nafasi hiyo kwa kuwa na viwanja vizuri sana na hasa walipoandaa mashindano ya Kombe la Dunia kwa mafanikio makubwa mwaka 2010.
Walipatiwa nafasi hiyo ya kuandaa Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 2013 baada ya Libya kuonekana isingeweza kutokana na ghasia zilizotokea nchini humo.
Miji tisa imearifiwa imejipanga kuandaa mashindano hayo ya mwakani yenye mvuto barani Afrika.
Miji inayopewa nafasi kubwa ni Johannesburg, Cape Town, Durban, Port Elizabeth, Polokwane, Nelspruit na Bloemfontein.
Viwanja katika miji hiyo vilitumika kwa michuano ya Kombe la Dunia na vitakuwa katika hali nzuri kuandaa mashindano ya kandanda ya bara la Afrika.
Fainali hizo za Kombe la Mataifa ya Afrika zinazoshirikisha nchi 16 zitaanza patashika zake kuanzia katikati ya mwezi wa Januari hadi katikati ya mwezi wa Februari mwaka 2013.

No comments:

Post a Comment