Pages

Thursday

Charles Taylor ahukumiwa miaka 50




















                              imeandikwa na sauti ya amerika
Mahakama maalumu kwa ajili ya Sierra Leone imemhukumu Rais wa zamani wa Liberia Charles Taylor kifungo cha miaka 50 jela kwa uhalifu wa vita na uhalifu dhidi ya binadamu.

Mahakama hiyo mjini The Hague ilitangaza uwamuzu huu na kusema Taylor alitumia nafasi yake kuwasaidia waasi badala ya kuhamasisha amani na uthabiti.

Jaji kiongozi Richard Lussick alisema hatua za Taylor za kusambaza silaha kuwahamasisha na kuwaelekeza waasi zinamulika kiwango cha uovu wa tabia yake ya uhalifu.

“Kwa kutoa kwake silaha bila ya kusita kuliongeza muda wa vita vya Sierra Leone na kuongeza uhalifu uliotokana na vita hivyo.”

Waendesha mashtaka waliomba apatiwe kifungo cha miaka 80 lakini mahakama ilisema kiwango cha hukumu hiyo kitakuwa cha kupita kiasi.

Mahakama ilimkuta na hatia Taylor mwenye umri wa miaka 64 mwezi uliopita kwa makosa yote 11 aliyokabiliwa nayo ambayo inajumuisha mashtaka ya mauaji, ubakaji, utumwa wa ngono, kuwapatia mafunzo wanajeshi watoto na utumwa.

Mahakama iligundua Taylor hakuwa na mamlaka na udhibiti wa waasi waliotenda maovu wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Sierra Leone lakini alifahamu kazi zao na aliwapatia silaha na vifaa vingine.

Ilieleza Jumatano kwamba nafasi ya Taylor kama kiongozi wa nchi yake inamuweka katika daraja la kipekee ikilinganishwa na wakosaji waliopatikana na hatia mapema na mahakama hiyo.

Taylor ni mkuu wa kwanza wa nchi kukutwa na hatia na mahakama hiyo ya kimataifa tangu kesi ya Nuremberg mwaka 1946 ya Karl Doenitz aliyetawala kwa muda mfupi Ujerumani chini ya mfumo wa Nazi baada ya kifo cha Adolf Hitler.

No comments:

Post a Comment