Pages

Friday

Kabila akataa shinikizo la ICC kumkamata Ntaganda




Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, Joseph Kabila anakataa shinikizo la kimataifa kumkamata jenerali mmoja wa jeshi anayetafutwa na mahakama ya kimataifa ya uhalifu-ICC,  kwa  mashtaka ya uhalifu wa vita.
Bwana kabila aliwaambia waandishi wa habari wakati wa ziara yake ya mashariki ya nchi hiyo siku ya jumatano, kwamba Bosco Ntaganda, atakamatwa, lakini kwa sababu ya watu wa Congo.

“Tutamkamata, tunasababu zaidi ya 100 za kumkamata na kumhukumu hapa, na ikiwa si Goma itakua Kinshasa au kwingineko. Hiyo sio sababu tunayokosa, na wananiambia kuhusu shinikizo litakalozidi kutoka jumuia ya kimataifa. Mimi ninafanya kazi kwa ajili ya wananchi wangu, kwa wacongo wote.”

ICC inamshtaki Ntaganda kwa mashtaka ya uhalifu wa vita uliofanyika wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo, ikiwa ni pamoja na kuwaandikisha watoto kuwa wapiganaji.  Wakati huo, Ntaganda alikuwa naibu kamanda wa kundi moja la kisiasa lenye silaha lililoitwa Union of Congolese Patriots.

Mkuu wa jeshi la Congo, Jenerali Didier Etumba, alikiri kwamba Bosco alihusika na mauaji yaliyofanywa chini ya uongozi wake  na alisema hawezi kulitumikia jeshi la Congo.

“Inabidi tukubali kwamba wanajeshi walikuwa wanamfuata kamanda wao, hivyo basi haikuwa hatua za wanaume hao, ni kamanda wao ambaye alitaka kuwatumia.”

Wiki iliyopita Ntaganda kiongozi wa zamani wa waasi, aliwaamrisha wanajeshi chini ya uongozi wake huko mashariki ya Congo,  kuasi na kusaidia kuimarisha  usalama wake binafsi. Rais Kabila alitembelea eneo hilo ili kuwashawishi wanajeshi  walioasi  kurudi jeshini.
Mkataba wa amani wa mwaka 2009 uliwataka waasi kujiunga na jeshi ya taifa nchini Congo.

No comments:

Post a Comment