Majaji wa Ufaransa wameomba kibali cha kimataifa ili waweze kumkamata mwanawe rais wa nchi yenye utajiri wa mafuta ya Equatorial Guinea.
Majaji wawili wanachunguza madai kwamba viongozi kadha kutoka barani Afrika wanamiliki mali nchini Ufaransa ambazo walinunua na pesa za serikali kutokana na ubadhirifu.Teodoro Nguema Obiang Mangue anasakwa kuhusiana na madai ya biashara ya pesa haramu.
Bwana Obiang, mtoto wa Rais Teodoro Nguema Obiang Mbasogo, amekanusha madai hayo.
Haifahamiki kama waendesha mashtaka wameidhinisha ombi la kutoa kibali cha kumkamata.
Majaji wa Ufaransa wanaochunguza tukio hilo Roger Le Loire na Rene Grouman wameomba kibali hicho baada ya serikali ya Equatorial Guinea kukataa kumhoji Bwana Obiang, ambaye anajulikana kama Teodorin nchini mwake.
Waandishi wa habari wanasema Teodorin Obiang, ambaye ni waziri wa kilimo wa serikali hiyo, anafahamika kwa kuishi maisha ya kifahari.
Olivier Pardo, wakili wa serikali ya Equatorial Guinea, ameliambia shirika la habari la Reuters kwamba uamuzi wa kuomba kibali cha kumkamata Teodorin "hauna msingi".
Mwezi uliopita, polisi walivamia nyumba moja katika eneo linaloishi watu matajiri mjini Paris kama sehemu ya uchunguzi wao, na kuchukua mivinyo na vitu vingine vyenye thamani ya mamilioni ya madola.
No comments:
Post a Comment