Pages

Friday

RAIS KIKWETE AMTEUA MBATIA

 



                                              Habari hii imeandikwa na Tanzania Daima

RAIS Jakaya Kikwete ameanza mchakato wa kuunda Baraza jipya la Mawaziri linalotarajiwa kutangazwa wakati wowote kuanzia leo huku akitoa taswira ya kuundwa kwa serikali itakayojumuisha wanasiasa wanaotoka nje ya Chama cha Mapinduzi (CCM).
Katika hatua ya kwanza, Rais Kikwete amewateua watu watatu wenye sifa na rekodi tofauti za kisiasa, kiuongozi na kitaaluma kuwa wabunge.
Miongoni mwa wateule hao watatu wapya wa Kikwete waliotangazwa jana ni Mwenyekiti wa Taifa wa chama cha NCCR-Mageuzi, James Mbatia.
Taarifa fupi ya Ikulu iliyosambazwa jana jioni kwa vyombo vya habari imewataja wengine walioteuliwa na rais kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania Ibara ya 66(i) (e) kuwa wabunge wapya ni pamoja na Prof. Sospeter Muhongo na Janet Mbene.

Kuteuliwa kwa Muhongo ambaye kitaaluma ni bingwa wa masuala ya jiolojia kuwa mbunge, kunaongeza uwezekano wa kuingizwa katika baraza la mawaziri akishika moja ya wizara nyeti.
Miongoni mwa wizara ambazo anaweza kushika kuziongoza ni pamoja na Wizara ya Nishati na Madini ambayo kwa sasa inaongozwa na William Ngeleja.
Wakati jina la Prof. Muhongo likiwa geni masikioni mwa Watanzania, uteuzi wa Mbatia ulizua mjadala wa ghafla kutoka kwa watu mbalimbali, akiwamo mmoja wa wabunge machachari wa NCCR- Mageuzi.
Hii ni mara ya pili kwa Rais Kikwete kuwateua wapinzani kuingia ndani ya Bunge. Alipata kufanya hivyo wakati alipokuwa akikaribia kumaliza muhula wake wa kwanza madarakani, wakati alipomteua kiongozi maarufu wa Chama cha Wananchi (CUF), Ismael Jussa Ladhu, kuwa mbunge.
Mbatia amewahi kuwa mbunge mwaka 1995-2000 kupitia chama hicho katika jimbo la Vunjo mkoani Kilimanjaro, ambapo katika uchaguzi ulioisha mwaka 2010 aliwania nafasi hiyo katika jimbo la Kawe na kuangushwa na mgombea wa CHADEMA, Halima Mdee.
Kuteuliwa kwa Mbatia kumefuta minong’ono ambayo ilikuwa ikimtaja Mwenyekiti wa Taifa wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, kuwa miongoni mwa wanasiasa wa upinzani ambao walikuwa wakipewa nafasi kubwa ya kuingia katika serikali mpya ya Kikwete.
Muhongo kitaaluma ni Profesa wa Jiolojia kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Kwa sasa ni Mhariri Mkuu Mtendaji wa jarida la jiolojia la kanda ya Afrika na vile vile ni mshirika wa wanajumuiya za kimataifa za wanataaluma wa jiolojia kama Geological Society of London na Chinese Academy of Geological Sciences.
Prof. Muhongo pia ni Makamu wa Rais wa Kamisheni ya wanajiolojia wa ramani ya dunia toka mwaka 2005 hadi sasa.
Amehudumu kama mtafiti katika Chuo Kikuu cha Mainze nchini Ujerumani mwaka 2000 hadi 2009.
Mwaka 2009, alikuwa miongoni mwa watu waliopendekezwa kutoka Tanzania kushika nafasi ya Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO).
Janet Mbene ambaye anateuliwa na Kikwete kwa mara ya pili katika mihula tofauti kuwa mbunge, ni msomi na mchumi wa ngazi ya juu akiwa amefanya kazi katika taasisi na mashirika mengi ya kimataifa.
Akiwa mwanzilishi na mkurugenzi wa taasisi ya SIA, inayojihusisha na kuwajengea uwezo wa kiuchumi kampuni ndogo na za kati hapa nchini, Mbene amewahi kufanya kazi katika shirika la kimataifa la Oxfam linalojihusisha kupambana na umasikini, chini ya mradi wa Maendeleo wa Umoja wa Mataifa na Shirika la Kazi duniani (ILO).
Katika nafasi hizo, Mbene ambaye hivi karibuni alianguka katika kinyang’anyiro cha ubunge wa Afrika Mashariki, alijikita zaidi kusimamia miradi ya maendeleo iliyolenga kuwasaidia wajasiriamali na wazalishaji wa bidhaa, masoko na kusimamia kikamilifu utendaji kazi bora za sekta binafsi.
Mbene ni mwanzilishi wa taasisi ya Yatima ambayo inalea watoto yatima ambao wazazi wao wamekufa kwa ukimwi na kupigania haki za yatima.
Aidha alianzisha bodi ya wadhamini ya wanawake wachumi Tanzania, yenye lengo la kuinua uwezo wa kiuchumi wa wanawake hususan wa vijijini.