WAZIRI Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye amelitaka Jeshi la Polisi nchini kuacha kutumia silaha za moto au nguvu ya ziada linapokabiliana na raia, badala yake litumie busara kutatua migogorobaada ya kufunga mafunzo wa wahariri wa vyombo vya habari yaliyohusu utawala, Sumaye alisema kufa mtu katika mapambano ya polisi na raia siyo kitu kidogo.
Kauli hiyo ya Sumaye inaonekana kuwalenga polisi ambao wanadaiwa kusababisha kifo cha aliyekuwa mwandishi wa habari wa Televisheni ya Channel Ten mkoani Iringa, David Mwangosi.
Mpaka sasa askari watano wa jeshi hilo, akiwamo anayetuhumiwa kumlipua kwa bomu marehemu Mwangosi, wamekamatwa na wanaendelea kuhojiwa na jeshi hilo mkoani Iringa.
Sumaye alisema kuwa katika siku za karibuni, polisi wamekuwa wakikimbizana na raia mara kwa mara pamoja na kutumia silaha na nguvu isiyo ya kawaida hata pale pasipostahili. Jambo ambalo alisema siyo sahihi kwa mustakabali wa jeshi hilo.
“Si lazima sana kwa polisi kutumia silaha hasa za moto kila wakati. Nimekuwa nikitazama kwenye televisheni mara kwa mara na kuona polisi wakitumia silaha, hata sehemu za kuvunja nyumba tu huko vijijini. Nawashauri watumie busara,” alisema Sumaye na kuongeza:
“Tusidhani risasi inaweza kutatua migogoro wakati wote. Risasi inaweza kuharibu kila kitu, zitumike pale inapokuwa ni lazima kwani Watanzania siku zote si watu wa fujo.”
Alisema kutokana na tukio la hivi karibuni la kuuawa kwa mwandishi wa habari, Serikali, Polisi na vyombo vingine vya usalama, watakuwa wamejifunza kitu katika kutatua migogoro na migongano baina yao na wananchi wanaowaongoza.
No comments:
Post a Comment