Pages

Monday

taarifa ya serikali ya mapinduzi zanzibar

 
Mohammed Aboud Mohammed,  Waziri wa Nchi,  Ofisi ya Makamu wa Pili              
                                            wa  Rais, Zanzibar.
---             
Itakumbukwa kwamba tarehe 25 Aprili, 2012 Kamati Maalumu ya Mawaziri ilikutana na viongozi wa jumuiya ya Uamsho, Maimamu na Masheikh kuzungumzia hali iliyojitokeza nchini katika kufanya mihadhara ambayo ilikuwa inaashiria uvunjifu wa amani.

Katika kikao hicho Serikali iliwataka Viongozi hao wanapofanya mihadhara na mikutano inayohusu masuala ya maoni ya katiba wafuate taratibu zilizowekwa kisheria.

Aidha, Serikali iliwasihi viongozi hao kuepuka matumizi ya lugha na vitendo vinavyoashiria uvunjifu wa amani katika nchi yetu na iliwataka pale ambapo wana maoni yoyote kuhusu Serikali wafuate taratibu zilizowekwa na Serikali itakuwa tayari kuzungumza nao ili kuwa na mustakabali mwema katika nchi yetu.

Vile vile, kupitia taarifa maalumu ya Serikali iliyotolewa Aprili-Mei mwaka huu, Serikali ilieleza wazi kwamba tume ya marekebisho ya katiba imezinduliwa rasmi na kuwataka wananchi, taasisi na vikundi mbali mbali nchini vyenye nia ya kutaka kuelimisha umma kuhusu marekebisho ya katiba kufuata muongozo wa sheria namba 8 ya mwaka jana kama ilivyorekebishwa na sheria namba 2 ya mwaka huu 2012.

Kwenda kinyume na sheria hii ni kosa la jinai na hivyo iliwataka Wananchi wote kujiepusha na vitendo vyote vinavyokwenda kinyume na matakwa ya sheria.

Ndugu Wananchi, mbali na juhudi hizo za Serikali, bado wapo watu wachache wasioitakia mema nchi yetu na umoja uliopo wanaendeleza kwa makusudi vitendo vya kuvunja taratibu za sheria jambo ambalo limepelekea Jeshi la Polisi kuchukua hatua za kisheria.

Ndugu Wananchi, Serikali imesikitishwa na vitendo vilivyojitokeza vya vurugu na uvunjifu wa amani ambavyo vimeelezwa kwa kina na Jeshi la Polisi iliyotolewa mapema leo tarehe 25.05.2012 na Kamishna wa Polisi Zanzibar.

Kutokana na hali hiyo, Serikali inawahakikishia Wananchi wote kwamba itaendelea kudhibiti vitendo vyovyote vya uvunjifu wa sheria vinavyoashiria kuondolea nchi yetu amani na utulivu uliopo.

Ndugu Wananchi, Serikali inawahakikishia Wananchi kwamba Jeshi la Polisi litaendelea kuchukua hatua zifaazo ili kuwahakikishia usalama wa raia na mali zao unakuwepo na hali inaendelea kuwa shuwari, amani na utulivu.

Ndugu Wananchi, bado Serikali inasisitiza na kuwaomba wananchi wote waunge mkono juhudi za Serikali na kuacha kabisa kujiingiza katika vitendo ambavyo vinaashiria uvunjifu wa amani na utulivu katika nchi yetu.

Hivyo, tunawaomba Wananchi waendelee na shughuli zao kama kawaida na Serikali itaendelea kuwahakikishia usalama wao.

Aidha, Serikali inawaomba wazazi kuwadhibiti vijana wao wasijiingize katika vitendo viovu na vurugu kwani Jeshi la Polisi na Vikosi vyote vya Ulinzi na Usalama vitakuwa macho kupambana na vurugu hizo na vitendo vyote vya uvunjifu wa amani.

Kwa madhumuni ya kudhibiti amani na utulivu na usalama wa Wananchi wetu, Serikali katika kipindi hiki itachukua hatua zifuatazo:
  1. Inakataza mikusanyiko ya aina mbalimbali, maandamano, na mihadhara ya aina mbalimbali ambayo haijapata kibali cha Serikali.
  2. Serikali inaliagiza Jeshi la Polisi kuwatafuta na kuwafikisha katika vyombo vya sheria wale wote waliohusika na kufanya fujo zilizotokea katika maeneo mbali mbali ya Zanzibar
  3. Serikali inakemea vikali vitendo vyote vya hujuma na uharibifu wa amali zilizofanywa katika taasisi za umma, dini na mali za watu binafsi.
  4. Serikali inawapa pole Wananchi na Taasisi zilizoathirika na vurugu hizo na kuwahakikishia kuwa hatua kali zitachukuliwa dhidi ya wale wote waliohusika katika kadhia hiyo.

Na mwisho, tunawaomba wananchi kushirikiana na Serikali kwa kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi pale ambapo itaonekana zipo dalili za uvunjifu wa amani katika maeneo yao.

Ahsanteni.

Nawashukuru kwa kunisikiliza.


Mohammed Aboud Mohammed, 
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, 
Zanzibar.

No comments:

Post a Comment