Pages

Wednesday

Kikosi cha AMISOM kimezindua kampeni kali dhidi ya wanamgambo wa Al-Shabab

 Vifaru vya AMISOM katika shughuli zake za kijeshi dhidi ya kundi la Al-Shabab nchini Somalia
                                  imeandikwa na sauti ya amerika
Vikosi vya Somalia kwa kuungwa mkono na majeshi ya Umoja wa Afrika yamezindua  kampeni kali  ya kutimua wanamgambo wa al-Shabab katika vitongoji vya Mogadishu  hususan kwenye ukanda wa Afgoye.

Maafisa wa ulinzi wanasema lengo la kampeni hiyo ni kuleta uthabiti  na amani kwa watu 400,000 waliofurushwa makwao katika eneo la Afgoye lililoko magharibi ya mji wa Mogadishu.  Hii ni mara ya kwanza vikosi vya Umoja wa Afrika  na majeshi ya kitaifa ya Somalia  kuungana pamoja kushambulia vituo vya wanamgambo wa al-Shabab nje ya Mogadishu.
Msemaji wa kikosi cha Umoja wa Afrika kinachojulikana kama AMISOM- Paddy Ankunda, aliiambia Sauti ya Amerika kuwa  kampeni dhidi ya al-Shabab ilizinduliwa katika wilaya ya Daynile na kuelekea magharibi mwa Mogadishu kuingia katika eneo la Afgoye.

Alisema wilaya ya Daynile sasa imo mikononi mwa majeshi ya AMISOM na kwamba wanapigania kijiji kidogo kiitwacho Elasha Biyaha kilichoko karibu na Afgoye na ripoti za hivi karibuni alizopata  ni kwamba majeshi ya Umoja wa Afrika  sasa yanadhibiti asilimia 85 ya kijiji hicho.

Eneo la Afgoye lina watu 400,000 waliofurushwa makwao kwenye eneo la kilomita 30 mraba kutoka mji mkuu wa Mogadishu. Ni mahala ambapo watu wengi  kutoka Mogadishu wamepiga kambi katika kipindi cha mwaka mmoja baada ya mji huo mkuu kushambuliwa kwa risasi kila siku katika mapigano baina ya  vikosi vya serikali na wanamgambo wa al-Shabab.

Mashirika ya kutoa misaada ya kibinadamu yameeleza wasiwasi wao juu ya raia wanaojeruhiwa  katika mtafaruku huo na kuziomba pande zote kuepuka kutumia nguvu na kupigana kiholela  ambapo raia wanajikuta wamenaswa kwenye mapigano hayo.

Vikosi vya Umoja wa Afrika vilifanikiwa kiasi kikubwa kutimua wanamgambo hao wa Kiislam mwaka jana mjini Mogadishu  na kuimarisha kwa kiwango kikubwa mji huo mkuu. Lakini eneo la Afgoye ni mojawapo ya maeneo yaliyobaki mikononi mwa wanamgambo wa al-Shabab.

Wanamgambo hao walilifanya eneo hilo kuwa ngome yao ambapo walikuwa wakiwaandikisha wanachama wapya na hata kuwapa mafunzo na pia kulifanya eneo kuwa la mkutano wa viongozi wake ambapo  wanaeneza propaganda zao.

No comments:

Post a Comment